Saturday, 26 September 2020

KILIMO BORA CHA MAHARAGE YA NJANO



Kilimo cha maharage ni rahisi na kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani kwako na kuchukua mzigo.

Ekari moja ya maharage ya njano kwa maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo unalolimia.

Shamba la maharage kama unalima kwa kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi minne.

Upandaji wa Maharage 


1.Mbegu. 
Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani.

Maji mengi yaliyotuama na ukame siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.

Kuna aina nyingi za maharage ambazo zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder) ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa wakulima ambazo huhimili

baadhi ya magonjwa na wadudu. 
Inashauriwa kupanda maharage katika umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.

Kama mbegu moja moja katika kila shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo idadi yake ni nusu ya maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 = ekari 2.471.

2. Mbolea.
Mimea huhitaji virutubisho kutoka kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage huhitaji madini ya ‘phosphorous’ na ‘potassium’ ambayo hupatikana kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo na mabaki ya mimea.

Ni muhimu kufahamu udongo ambao unatarajia kupanda mimea yako ili kutathmini viwango vya madini yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza.

Zaidi ya yote ni vizuri kutumia mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen. Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye udongo.

3.Magugu. 
Inashauriwa kupalilia mimea kabla haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza kusababisha magonjwa kwa mmea.

Inashauriwa kupanda mimea kwa kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza kushambulia
mimea.

4.Wadudu na magonjwa. 
Maharage hushambuliwa na wadudu na magonjwa. Miongoni mwa njia za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu ni kuhakikisha kuwa mimea ipo katika hali nzuri (imepaliliwa, nafasi ya kutosha na haijaharibika).

Pia kubadilisha aina ya mimea inayopandwa kwenye shamba moja mara kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa wadudu kuongezeka. Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi (African Ballworm) huweza kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au vitunguu saumu.

Maji ya muarobaini ni dawa nzuri sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa binadamu.

5.Kukomaa na Kuvuna.
Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda. Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka kinapokuwa kimefikiwa.

Kwa mfano asilimia 80 ya maharage yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.

Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.

Baada ya kukauka hadi kufikia angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha kuyafunika tena.

6. Kilimo mchanganyiko. 
Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.

Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous) kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi weupe.
Share:

KILIMO CHA TANGAWIZI



Tangawizi ni aina ya zao la kiungo ambalo sehemu inayotumika ni tunguu (rhizome) ambalo huonekana kama mizizi ya mmea. Asili ya zao hili ni maeneo ya kitropiki ya bara la Asia na hasa katika nchi za India na China.

Zao hili linazalishwa kwa wingi kutoka katika nchi ya Jamaica. Hapa nchini zao hili hulimwa katika mikoa ya Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Kilimanjaro.

Tangawizi hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji (kama chai, soda, juisi, vilevi n.k) na vyakula mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga, achari n.k. Hutumika pia katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi n.k. pia hutumika katika vipodozi kama poda n.k).



AINA ZA TANGAWIZI 
Hakuna uthibitisho wa aina za tangawizi ambazo hulimwa hapa nchini ila kuna dalili ya kuwa na aina za White Africa (Jamaica) na Cochin (flint); hii huwa na tunguu ngumu zenye nyuzi.

TABIA YA MMEA 
Tangawizi ni mmea unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu ya ardhi. Jamaica ina rangi hafifu ya kahawia na tunguu fupi wakati Cochin ina tunguu fupi zaidi lenye ngozi ya rangi iliyo kati ya kijivu na nyekundu. Mmea una urefu wa futi mbili na majani yake ni membamba marefu ambayo hufa kila mwaka yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua ya mmea huu yana rangi nyeupe au manjano.




HALI YA HEWA NA UDONGO 
Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha mm.1,200-1,800 na joto la wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25. Hustawi vema katika udongo tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.




MMEA WA TANGAWIZI



UPANDAJI 
Zao la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu vyenye kichipukizi kizuri angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sm.2.5-5. Wakati mwingine, vichipukizi vinavyopatikana katika kumenya tangawizi huweza kuhifadhiwa na kutumika kwa kupanda. Kiasi cha kilo 840-1700 cha vipande vya tunguu huweza kutumika kwa kupanda katika hekta moja. Nafasi inayotumika kupanda ni kati ya sentimita.23-30 kwa 15-23 na kina cha sentimita.5-10 na mara nyingi hupandwa katika matuta. Baadhi ya mazao huweza kupandwa katika shamba la tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa si lazima kivuli kiwepo. Inashauriwa kumwagilia maji endapo mvua inakosekana.

Wiki 1-2 kabla ya kupanda weka mbolea ya samadi au mboji kiasi cha tani 25-30 kwa hekta na kwa kukuzia weka kiasi cha NPK kwa uwiano wa kilo 36:36:80. Tandaza nyasi shambani kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapokosekana. Palizi hufanywa mara magugu yanapoota, dawa ya kuua magugu, kama simazine au round up hutumika.




Magonjwa na wadudu: 


Madoa ya majani yanayosababishwa na viini vya magonjwa viitwavyo Colletotrichum zingiberis na Phyllosticta zingiberi.
Kuoza kwa tunguu; kunasababishwa na viini viitwavyo Pithium spp
Mizizi fundo; inasababishwa na Meloidegyne spp.





UVUNAJI 
Tangawizi huweza kuwa tayari kwa kuvuna kati ya miezi 9-10 baada ya kupanda, wakati majani yake yanapogeuka rangi kuwa njano na mashina kusinyaa. Tangawizi inayohitajika kwa kuhifadhi kwenye kemikali (preserved ginger in brine) huvunwa kabla haijakomaa kabisa, wakati ile iliyokomaa kabisa huwa kali zaidi na huwa na nyuzi hivyo hufaa kwa kukausha na kusaga. Mavuno hutofautiana kulinganana na huduma ya zao, mavuno yanaweza kuwa kiasi cha tani 20-30 cha tangawizi mbichi huweza kupatikana.




USINDIKAJI 
Tangawizi ikisindikwa utapata unga, mafuta maalum (essential oils) n.k. Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa, kukatwa na kukaushwa juani au mara nyingine huchovywa katika maji yaliyochemka kwanza na ndipo kukaushwa au hukamuliwa mafuta. Pia tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa zimechanganywa na sukari na/au chumvi au bila kuweka kitu chochote. Hata hivyo tangawizi ina Kiasi cha mafuta cha 16.0-18.0%
Share:

Popular Posts

Copyright © LUMBIJI KWETU | Powered by Blogger Design by Yuvinusm